Total Pageviews

Monday, July 9, 2012

QUEEN OF THE GORILLAS(MALKIA WA MASOKWE-22)

WAKATI nyota ya jaha ikianza kumuwakia Harvey, kijana mdogo mwenye asili ya nchini Liberia aliyepitia kipindi kigumu sana maishani mwake kutokana na machafuko ya kisiasa nchini kwao yaliyozigharimu roho za wazazi na ndugu zake, kikwazo kingine kikubwa kinaanza kujitokeza.
Mtoto wa Dk Lewis, mwanaume wa makamo aliyempokea Harvey na kujitolea kuyabadilisha maisha yake aitwaye Skyler, anaanza kuonesha hisia za mapenzi kwa kaka yake huyo wa hiyari. Anatumia mbinu mbalimbali kuwasilisha ujumbe wake wa kimapenzi kwa Harvey lakini anakuwa mjanja na kujitahidi kuvishinda vishawishi.
Bado Skyler hakati tamaa na anajiapiza kuwa atafanya kila linalowezekana kuhakikisha analipata penzi la Harvey, ambaye sasa umaarufu wake ulikuwa ukizidi kuongezeka siku baada ya siku, kutokana na kiwango kikubwa cha kucheza mpira wa kikapu alichokionesha kwenye mashindano ya NCAA, yaliyokuwa yanawahusisha wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali nchini Marekani.
Je, nini kitafuatia? Skyler atafanikiwa kumnasa Harvey? Itakuwaje?
SONGA NAYO...
HARVEY alifungua boksi la zawadi, akakutana na harufu nzuri ya manukato yaliyokuwa yamepuliziwa vizuri. Akaanza kutoa zawadi moja baada ya nyingine. Kwa kiasi fulani alifurahishwa na zawadi zile, akajilazimisha kuamini kuwa kwa sababu zimetoka kwa dada yake, hakutakuwa na tatizo lolote.
“Umezipenda?”
“Nimezipenda sana Skyler, nashukuru kwa kunijali.”
“Hizo zinakutosha? Hebu ijaribu hata moja nione inavyokupendeza,” alisema Skyler huku akinyoosha kidole kwenye nguo za ndani alizokuwa amemletea Harvey kama zawadi.
“Nitazijaribu nikiwa peke yangu… naamini zitanipendeza sana,” alisema Harvey akiwa tayari ameshaugundua mtego wa Skyler.
“Hapana bwana, mi’ nataka uzijaribu sasa hivi ili nione kama nimechagua nzuri,” alisema Skyler na kusimama, akamsogelea Harvey na kuushika mkanda wa suruali yake, akawa anajaribu kuufungua lakini Harvey akatumia ujanja wa hali ya juu.
“Subiri kwanza nikazibadilishie bafuni halafu nitakuita uje unione nilivyopendeza,” alisema Harvey na kuzichukua, akaelekea kwenye bafu lililokuwa ndani. Alipofika aliingia na kujifungia mlango kwa ndani, akawa anahema juujuu huku akifikiria namna ya kumkwepa Skyler.
“Kwani akiniona nitapungua nini, potelea mbali, liwalo na liwe,” alisema Harvey huku akianza kuivua suruali yake na kuzijaribu zile nguo za ndani alizoletewa na Skyler. Wakati akiendelea kubadilisha, alisikia sauti ya mwanachuo mwenzake, Cazzard akimuita na kugonga mlango.
“Nipo huku bafuni, nakuja,” alisema Harvey huku moyoni akishukuru kwa kitendo cha rafiki yake huyo kumfuata. Harakaharaka alivaa suruali yake na kutoka, akamfungulia mlango. Alipomtazama Skyler, alimuona akikunja sura kuashiria kuwa hakufurahishwa na ujio wa Cazzard.
“Nimetumwa kuja kukuita, kuna wageni wako pale utawala,” alisema Cazzard, Harvey akaweka vitu vyake vizuri na kuzifungia zile zawadi zake kwenye kabati.
“Twende mara moja halafu tutarudi kuja kuendelea,” alisema Harvey huku akimshika mkono Skyler na kumuinua, kwa shingo upande akakubali kuongozana naye. Walikwenda mpaka kwenye ofisi za utawala wa chuo kile ambapo Harvey aliwaona wanaume wawili waliokuwa wamevalia suti nadhifu na kubeba ‘briefcase’ mikononi mwao. Aliwakumbuka vizuri kuwa ni wale maofisa wa timu ya Miami Heat, akatabasamu.
Aliwasalimu kwa heshima, wakaenda kukaa kwenye chumba cha mazungumzo ambapo walianza kumuuliza juu ya hatua aliyofikia kuhusu mkataba waliomuachia siku iliyopita. Aliwajibu kuwa kila kitu kilienda vizuri, akawaomba wamsubiri kidogo akaulete ukiwa tayari umeshajazwa. Skyler naye alisimama, wakaongozana hadi kwenye hosteli ya akina Harvey.
“Nina furaha sana Skyler, wale ndiyo mameneja wa Miami Heat walioleta ule mkataba niliokuja nao jana nyumbani, naamini siku chache zijazo na mimi nitakuwa mchezaji maarufu sana duniani,” alisema Harvey kwa furaha akitegemea Skyler atamuunga mkono lakini haikuwa vile.
“Wee ukishakuwa maarufu si utatafuta wanawake wengine maarufu kama wewe? Mi’ sitaki uwe maarufu,” alisema Skyler huku akijikamua machozi, Harvey akamsogelea na kuanza kumbembeleza. Skyler aliitumia vyema nafasi ile kwani alijilaza kwenye kifua cha Harvey kwa kudeka, mikono yake akaipitisha kijanja na kuanza kumpapasa mgongoni.
“Harvey… nifanye nini ili uelewe hisia za moyo wangu? Nakupenda sana na nakuhitaji uwe wangu wa maisha,” alisema Skyler huku akizidi kumpapasa Harvey mgongoni.
“Nakupenda pia Skyler lakini hatuwezi kuwa wapenzi, sisi ni ndugu… tafadhali naomba unielewe dada’angu.”
“Ndugu? Kwani mimi na wewe tumezaliwa tumbo moja? Halafu si nilishakukataza kuniita dada? Harvey nakuomba utibu maradhi ya moyo wangu, naomba unielewe… Nakupenda sana,” alisema Skyler kwa sauti iliyojaa huba, akamsogezea mdomo wake na kutaka kumbusu lakini Harvey akamkwepa na kumwambia kuwa wafanye haraka kwa sababu wanasubiriwa na watu muhimu kule nje.
“Kwa hiyo hao mameneja wa Miami Heat ni muhimu kuliko mimi? Kwa nini hutaki kunielewa Harvey? Nifanye na mimi nijione ni mwanamke niliyekamilika, naomba niwe mpenzi wako,” alilalama Skyler huku akizidi kumkumbatia Harvey kwa nguvu.
Harvey aliamua kutumia nguvu kumtoa Skyler mwilini mwake. Akaenda kwenye kabati lake la kuhifadhia vitu na kuutoa ule mkataba ambao tayari ulishajazwa. Akamuinua Skyler ambaye alikuwa amejiinamia huku akilia, akampa moyo kuwa suala lile watalijadili kwa kina baada ya kumaliza taratibu za kukabidhiana ule mkataba na maafisa wa Miami Heat.
Skyler alikubali kwa shingo upande, wakatoka na kurudi kule utawala ambapo waliwakuta wale maafisa wa Miami Heat wakiwasubiri. Alipowapa mkataba uliojazwa, walimpa kitabu maalum cha kusaini kisha mmoja akafungua briefcase yake na kutoa hundi.
“This cheque worth ten thousand dollar for you! Registration allowance,”
(Hundi hii ina thamani ya dola elfu kumi kwa ajili yako! Posho ya usajili)
alisema afisa mmoja huku akiigeuza na kuisaini upande wa nyuma. Kwa Harvey, ule ulikuwa kama muujiza. Dola elfu kumi kama posho, nje ya malipo ya mkataba na mshahara wake, hakutaka kuamini haraka. Baada ya makabidhiano yale, wale maafisa waliaga na kuondoka, wakamuahidi kuwa watawasiliana naye na kumpa maelekezo ya nini cha kufanya baada ya kusaini mkataba.
Kwa furaha aliyokuwa nayo Harvey, alijikuta akimkumbatia Skyler kwa nguvu, akambusu kwenye paji la uso wake na kumnyanyua juujuu. Kitendo kile angalau kilirejesha furaha kwenye mtima wa Skyler. Wakakubaliana kuwa waondoke asubuhi ileile mpaka benki kwa ajili ya kwenda kuzitoa fedha zile.
“Nisubiri hapahapa nikajiandae, nakuja muda si mrefu,” alisema Harvey, akaondoka mbiombio hadi chumbani kwake ambapo alibadilisha nguo tayari kwa kutoka kwenda kuchukua fedha zake benki. Muda mfupi baadaye, tayari alishakuwa amejiandaa.
Wakaondoka na Skyler mpaka kwenye benki kubwa ya Miami Corporate, Harvey akatoa ile hundi na taratibu za kibenki zikaendelea. Baada ya muda mfupi, noti mpya za dola miamia zilipangwa mbele ya Harvey, akazichukua na kuzihakiki kisha wakaondoka na Skyler mpaka nyumbani kwao.
“Si umefurahi sana Harvey.”
“Nimefurahi mno Skyler, yaani hata sijui niseme nini,” alijibu Harvey bila kuelewa sababu za Skyler kumuuliza vile, akamshika mkono na kumwambia amfuate.
“Unataka kunipeleka wapi?”
“Wee nifuate bwana, unaogopa nini,” alisema Skyler huku akizidi kumvuta Harvey mkono, akampeleka mpaka chumbani kwake na kumsukumia kitandani, akafunga mlango kwa funguo kisha akazitupia chini ya kitanda.
“Kwa kuwa leo umefurahi nataka na mimi unifurahishe, nimechoka kuteseka kwa ajili yako,” alisema Skyler huku akianza kutupa nguo mojamoja mwilini mwake. Akavua gauni lake zuri alilokuwa amelivaa na kubakia na nguo za ndani. Umbo lake changa likajionesha vizuri mbele ya Harvey.
“Sijawahi kumruhusu mwanaume yeyote kuujua mwili wangu, nilikutunzia wewe hii zawadi, naomba uitumie na mimi nijione ni mwanamke niliyekamilika,” alisema Skyler huku akijinyonganyonga kiuno chake kama dondora na kurembua macho yake kimahaba. Harvey alikuwa ameduwaa pale kitandani akiwa ni kama hayaamini macho yake. Taratibu uzalendo ukaanza kumshinda, hisia za mapenzi zikaanza kumpanda.
Je, nini kitafuatia? Usikose siku ya Ijumaa kwenye gazeti la Ijumaa.

No comments:

Post a Comment